Tuesday, May 26, 2015

DHANA YA NENO

DHANA YA NENO NI TATA

Na Mwl.  CLEMENT, D.L



SWALI:  Baadhi ya wanaisimu wanakubaliana kwamba dhana ya neno ni tata. Pinga au kubali
                kauli hii kwa hoja madhubuti.


Katika kueleza dhana ya neno ni vyema  tukaanza na kutazama dhana ya mofolojia kwa ufupi. Dhana ya mofolojia imeelezwa na wataalam mbalimbali na miongoni mwao ni:
Habwe na Karanja (2012) wanadai kuwa mofolojia ni neno linalotumiwa kumaanisha utanzu wa isimu unaoshughulikia muundo wa maneno.
Hartman (1972) anaeleza kuwa mofolojia ni tawi la isimu ambalo hushughulikia uchunguzi na uchambuzi wa maumbo na aina za maneno yaliyo pamoja na historia zake.
Hivyo baada ya kuona fasili hizo kulingana na wataalamu mbalimbali, mofolojia yaweza kufasiliwa kama taaluma ya isimu inayojishughulisha na uchunguzi, uchambuzi na ufafanuzi wa maumbo ya maneno. Baada ya kuona fasili mbalimbali za mofolojia kulingana na wataalamu mbalimbali na kisha kuona fasili ya ujumla, sasa kwa ufupi tuitazame dhana ya neno. Dhana ya neno imefasiliwa na wataalamu mbalimbali na miongoni mwao ni hawa wafuatao:
Mdee (2010) anaeleza kuwa neno ni mfululizo wa herufi zilizofungamana pamoja na kuzungukwa na nafasi tupu.
Rubanza (2010) anadai kuwa neno kiothografia ni mfuatano wa maandishi ambao huacha nafasi tupu mwishoni bila uwepo wa nafasi tupu katikati.
Katamba (1994) anaeleza kuwa neno ni kipashio kidogo cha maana katika lugha ambacho kina dhima ya kisarufi. Anaendelea kusema, neno linaweza kusimama pekeyake na kuleta maana bila kupachikwa vipande vingine.

Ni kweli kuwa dhana ya neno ni tata katika kuifasili. Utata huu unatokana na vigezo mbalimbali vya kisarufi ambavyo wanaisimu huvitumia kama mwongozo katika kufasili dhana hii. Miongoni mwa vigezo hivyo ni kama ifuatavyo:

Wanaisimu wanatumia kigezo cha kiothografia. Katika kigezo hiki, huchukulia dhana ya neno kuwa ni maandishi yanayoacha nafasi mwisho. Neno hudhihirika katika maandishi tu na lisiwe na nafasi katikati. Kwa mfano Rubanza (2010) anaeleza kwamba neno kiothografia ni mfuatano wa maandishi ambao huacha nafasi tupu mwishoni bila uwepo wa nafasi tupu katikati. Kwa mfano katika sentensi; baba analima shambani. Katika mfano huu, sentensi tajwa ina maneno matatu yaliyopigiwa msitari. Kigezo hiki kina changamoto zifuatazo:
Kigezo hiki huchukulia maneno ambatani kuwa ni maneno tofauti kwa kuwa baadhi yake huandikwa kwa kuacha nafasi tupu katikati. Dai hili sio kweli kwasababu maneno ambatani hurejelea dhana moja hivyo hupaswa kuchukuliwa kama neno moja. Kwa mfano maneno kama: bata mzinga na bwana misitu.
Nafasi tupu huonekana katika maandishi tu (lugha ya maandishi) na hivyo kwa kiasi kikubwa kigezo hiki kimejikita zaidi katika lugha ya maandishi na kutupilia mbali lugha ya mazungumzo kwani tunapoongea nafasi tupu huwa hazionekani. Hali hii inapelekea kujiuliza maswali kama, je neno ni lile lililoandikwa tu?

Wanaisimu wanatumia kigezo cha kimofolojia. Katika kigezo hiki huchukulia kuwa, neno ni kipande cha lugha kinachotokana na kujengwa na kipashio kidogo cha kimatamshi kufuatana na vigezo au utaratibu fulani uliowekwa. Utaratibu huo hutofautiana kutoka lugha moja na nyingine. Kwa mfano Rubanza (2010) anaeleza kwamba zipo lugha ambazo upo uwezekano wa kulitambua neno kwa kutumia sifa za kimatamshi. Lugha kama hizi ni zile ambazo zina utaratibu wa kuweka mkazo mahali fulani maalumu katika maneno wakati wote. Anaeleza zaidi kwamba sehemu hiyo inaweza kuwa mwanzoni mwa kila silabi ya kwanza ya neno au silabi ya pili toka mwisho kwa baadhi ya lugha. Kwa mfano katika lugha ya Kiingereza sentensi “ I didn’t take the test yesterday”. Kutokana na utaratibu wa lugha hii ambapo mkazo huwekwa katika maneno yenye kubeba maana ya msingi (content words), sentensi hii ina maneno matatu yaliyokolezwa.
Utaratibu huu si mara zote kwani kuna wakati mwingine kutokana na sababu za kimsisitizo, maneno yanayobeba maana za kisarufi (grammatical words) huwekewa mkazo. Kwa mfano katika sentensi ileile mkazo ukiwekwa katika ‘I’ huonesha msisitizo kuwa sio yeye, ‘didn’t’ hakufanya na ‘the’ husisitiza jaribio hilo linalokusudiwa na muulizaji. Katika lugha ya Kiswahili mkazo huwekwa katika silabi ya pili kutoka mwisho. Kwa mfano ana'cheza, ana'lima na ana'kula.
Kigezo hiki kinasaidia kutofautisha maneno kwa kutumia mkazo hususa ni katika lugha ambazo mkazo huwa na uamilifu wa kubadili maana au kategoria ya neno. Kwa mfano katika lugha ya Kiingereza maneno kama: 'respect (nomino), res'pect (kitenzi) na 'record (nomino), re'cord (kitenzi) . Pia kigezo hiki kinatambua maneno katika lugha ya mazungumzo. Pamoja na ubora huu kigezo hiki kinakumbana na changamoto kadha. Miongoni mwa changamoto hizo ni:
Kigezo hiki kinashindwa kuweka bayana neno hasa ni lipi kwani tunaona kuna baadhi ya vipande-lugha visivyobeba maana ya msingi kama vile viunganishi na vihusishi katika lugha ya Kiswahili ambavyo haviwekewi mkazo. Swali ni kwamba, je vipande lugha hivyo ni maneno au si maneno?

Wanaisimu wanatumia kigezo cha kilekisika. Hiki ni kigezo kingine kinachotumiwa na wanaisimu kufasili dhana ya neno. Katika kigezo hiki, hueleza kuwa neno ni kipashio dhahania cha kilekisika ambacho huweza kudhihirika kimaana na kikazi. Kipashio hiki huweza kuwakilishwa kimaandishi au kimatamshi. Kwa mfano Mdee (2010) akimrejelea Crystal (1980) anaeleza kuwa leksimu ni kipashio dhahania kinachowakilisha maumbo kadhaa yanayotokana nacho. Kwa mfano: REFU- ndefu, mrefu, na kirefu. Kigezo hiki kina changamoto zifuatazo:
Hakiweki bayana juu ya maumbo yanayotokana na leksimu moja (midhihiriko ya hiyo leksimu) kuwa ni maneno tofauti au ni neno moja.
Kuna maneno yenye umbo moja lakini huwa na maana tofauti, je nayo yatakuwa ni neno moja au ni maneno tafauti? Kwa mfano maneno kama:
                      Paa        la nyumba (sehemu ya juu ya nyumba)
                                    mnyama
                                    enda juu au angani.
                        Mbuzi              mnyama
                                                kifaa cha kukunia nazi. 
  
Kigezo cha maana pia ni kigezo kingine ambacho wanaisimu mbalimbali hukitumia katika kufasili dhana ya neno. Katika kigezo hiki wanaisimu husisitiza maana katika kufasili dhana hii kwa kudai kuwa neno ni lazima liwe na maana. Kwa mfano Mdee (2010) anaeleza kwamba neno ni kipashio kidogo cha lugha chenye maana. Anaeleza zaidi kwamba neno ni lazima liwe na maana. Kwa mfano:  baba –  mzazi wa kiume, na mama – mzazi wa kike. Kigezo hiki pia kinakumbana na changamoto na miongoni mwa changamoto hizo ni kama ifuatavyo:
Kigezo hiki hakibainishi kuwa ni maneno yapi hulengwa hasa kwani kwa kiasi kikubwa kinaonekana kuegemea zaidi katika maana ya kilekisika na hivyo kuyasahau maumbo yenye maana za kisarufi kama vile viunganishi na vihusishi katika lugha ya Kiswahili.
Hakiweki wazi juu ya maneno yenye maana ya mficho kwa mfano nahau ambazo huundwa na umbo zaidi ya moja ilihali yakirejelea dhana moja. Kwa mfano:
                        mkono wa birika – mchoyo
                        pata jiko – kuoa.
Pia yapo maneno yenye maana zaidi ya moja kama vile: kaa, paa na kata. Maneno haya yakisimama pweke (peke yake), huwezi kupata maana moja hivyo ni lazima yawe katika mahusiano na maneno mengine matika mfumo wa matumizi katika sentensi ndipo upate maana. Mbali na kuwa katika mahusiano na maneno mengine katika sentensi, ni  muhimu pia kuzingatia muktadha ili kupata maana au dhana kamili ya maneno hayo.

Pia kigezo cha kisarufi ni miongoni mwa vigezo wanavyotumia wanaisimu katika kufasili dhana ya neno. Kwa mfano katamba (1994) anaeleza kuwa ili neno litambulike ni lazima liwe katika muktadha wa matumizi. Anaendelea kusema kuwa pia neno moja linaweza kuwa na dhima mbalimbali na dhima hizo hutambulika tu litakapokuwa ndani ya muktadha wa matumizi kwenye sentensi. Katamba (ameshatajwa) anatoa mfano wa neno la kiingereza ‘cut’ kwamba likiwa kiupweke, huwezi kutambua linarejelea nini. Neno hili linaweza kurejelea dhana tofauti linapokuwa katika mfumo. Kwa mfano;
i)                    ‘I need my cut’  nahitaji stahiki yangu (tafsiri ni yetu)
ii)                  ‘I have cut my finger’ nimekata kidole changu (tafsiri ni yetu)
Katika mifano hapo juu tunaona kuwa neno ‘cut’ katika sentensi ya kwanza limetumika kama nomino na katika sentensi ya pili kama kitenzi. Pia kigezo hiki kinaenda mbali zaidi katika kufafanua maumbo kama: na, tu na si (katika Kiswahili) na maumbo kama: and, an, the, na on (katika lugha ya Kiingereza) kuwa hutambulika yanarejelea nini au yana maana gani yakiwa katika muktadha wa matumizi.
Changamoto ya kigezo hiki ni kwamba si lazima maneno yote yawe katika muktadha wa matumizi ndipo tuweze kubaini maana zake kwani kuna baadhi ya maneno huweza kutambulika kuwa yana maana gani hata yasipokuwa katika muktadha  wa matumizi katika sentensi. Kwa mfano nomino za mahali kama vile: Dodoma, Mwanza na Morogoro na majina ya watu kama vile: Amina, Omari, Fatuma na Ali.

Mbali na vigezo wanavyovitumia wanaisimu katika kufasili dhana ya neno, wanakubaliana kuwa dhana ya neno ni tata hata katika uainishaji wa aina za maneno kiidadi na istilahi wanazozitumia. Kwa mfano katika kigezo cha idadi, Nkwera (1989) na Kapinga (1983) wanaainisha aina saba za maneno wakati Kihore (1969) anaainisha aina nane za maneno. Pia kiistilahi Nkwera (ameshatajwa), anatumia istilahi nomino wakati Kihore na Kapinga (wameshatajwa), wanatumia istilahi majina kurujelea dhana ileile.

Kwa kuhitimisha, katika kufasili dhana ya neno ni vyema kuzingatia vigezo vyote vya kisarufi kama vile othografia, fonolojia, sarufi, maana na lekisika ili kupunguza changamoto zinazojitokeza katika kufasili dhana hii kama ilivyojibainisha hapo juu. Hivyo kulingana na vigezo tajwa hapo juu dhana ya neno yaweza kufasiliwa kama kipashio cha lugha kilichojengwa na vipande sauti mbalimbali vya matamshi, chenye maana aidha ya kilekisika au ya kisarufi, kinachoweza kujibainisha kimaandishi na kimatamshi na kuwa na uwezo wa kuchukua sifa mbalimbali kinapokuwa katika muktdha wa matumizi.




MAREJEO
Habwe, J. & Karanja, P. (2012). Misingi ya Sarufi ya Kiswahili. Nairobi: Phoenix Publishers.
Katamba, F. (1993). Morphology. London: MacMillan Press Ltd.
Mdee, S. (2010). Nadharia na Historia ya Leksikografia. Dar es Salaam: TUKI.
Nkwera, F.V.M. (1989). Sarufi na Fasihi Sekondari na Vyuo. Dar es Salaam: Printpak.
Rubanza, (2010). Basic Reading.



12 comments:

  1. Asante kaka kwa matini yako niliyoielewa kwa usahihi zaidi

    ReplyDelete
  2. Shukran, umenirahisishia kazi

    ReplyDelete
  3. Naamini uwepo wenu japo nimeshindwa kuelewa kigezo cha kisarufi kina tofauti gani na hayo matawi mengine ya sarufi.

    ReplyDelete
  4. Asante xana ila sijaelewa apo kwenye isim na matawi mengine

    ReplyDelete
  5. alots of thanks to article writter because we are aware of many things now compared to before👍👍👍👍

    ReplyDelete
  6. Hongera nakala yako Ni nzuri Sana umenifanya nipate kuelewa kwa undnai Nini maana ya neno kwa vigezo mbali mblai utiwe nguvu ili uweze kuandika makala nyingi zaidi na zaidi.

    ReplyDelete