Friday, May 29, 2015

UAINISHAJI WA NGELI ZA NOMINO KWA KUTUMIA KIGEZO CHA KIMOFOLOJIA



Swali. Kwa kutumi mifano ainisha ngeli za nomino za Kiswahili kwa kigezo cha kimofolojia kisha
           jadili upungufu wa uainishaji huo.

Istilahi Ngeli imechukuliwa kutoka ligha ya kihaya (Tanzania). Katika lugha ya kihaya neno ngeli lina maana ya aina ya kitu.
Tuki (1990), wanaeleza kuwa Ngeli za nomino ni kundi moja la majina yaliyo na upatanisho wa kisarufi unaofanana na viambishi vya umoja na wingi vinavyofanana. Kwa mujibu wa fasili hii ngeli za nomino ni kundi la nomino zilizo na:
·         Upanisho wa kisarufi unaofanana (kisintaksia), na
·         Viambishi vya umoja na wingi vinavyofanana (kimofolojia).
Kamusi ya Kiswahili sanifu (1981), inaeleza kuwa ngeli za nomino ni utaratibu wa taaluma ya sarufi ya lugha katika kupanga aina za majina. Fasili hii ina upungufu kwa sababu tunaamini kuwa ngeli ni kundi la nomino za aina moja na ndio ule utaratibu wa kupanga nomino katika makundi kama fasili ya hapo juu inavyodai.
Kwa ujumla ngeli za nomino ni utaratibu unaotumika kupanga nomino za lugha katika makundi mbalimbali kwa kufuata vigezo vya kisarufi katika lugha ya kiisimu.
Kigezo cha kimofolojia ni kigezo ambacho huzingatia zaidi viambishi awali vya umoja na wingi lakini mzizi na viambishi tamati havihusishwi. Nomino zilizo na viambishi vya mwanzo vilivyosawa huwekwa katika ngeli moja. Ngeli za nomino huwa na sehemu mbili kimuundo ambazo huwa ni mwanzo na shina. Mwanzo huwa ni kiambishi awali na shina hujumuisha mzizi wa neno na kiishio ambacho huwa ni mofimu inayotumiwa kuunda nomino. Kiambishi awali ambacho hutumika kuainishia ngeli huitwa kiambishi ngeli.
Kwa kutumia kigezo cha kimofolojia ngeli za nomino za Kiswahili zimeainishwa katika makundi mbalimbali kwa kurejelea hali ya umoja na wingi wa nomino husika. Katika kigezo hiki kila kiambishi ngeli hupewa namba ya kukitambulisha. Kigezo hiki kimejadiliwa na wataalamu mbalimbali na miongoni mwao ni Mgullu na Habwe na Karanja.
Kwa kuanza na Mgullu (2001), katika kuainisha ngeli za nomino anazingatia zaidi viambishi awali vya idadi ya umoja na wingi katika nomino hizo. Mzizi na viambishi tamati katika nomino hizo huwa havihusishwi hata kidogo. Aidha viambishi awali vinavyotumika ni vile vya umbo la kawaida la nomino siyo viambishi awali vya ukubwa au udogo wa nomino hizo. Ngeli tutakazopata hapa zitakuwa ngeli za nomino za kimofolojia tofauti na ngeli za nomino za kisintaksia. Kwake yeye kundi moja la nomino zilizo na viambishi awali vya umoja na/au wingi vinavyofanana au nomino zilizo na viambishi awali hata kimoja huwa na ngeli yao. Yeye aliainisha makundi makuu manne ya ngeli za nomino kimofolojia ambayo ni; ngeli sita za nomino zilizo na viambishi awali vyote viwili yaani umoja na wingi, ngeli moja ya nomino zilizo na kiambishi awali cha umoja tu pamoja na mofu kappa ya wingi, ngeli moja ya nomino zilizo na kiambishi awali cha wingi tu pamoja na mofu kapa ya umoja, na ngeli moja ya nomino zisizo na kiambishi chochote. Kwa ujumla anaainisha ngeli za nomino tisa ambazo ni kama ifuatavyo:
1)      Ngeli ya MU-WA
Katika ngeli hii zipo nomino zilizo na kiambishi awali {MU} katika umoja na kiambishi awali {WA} katika wingi. Kwa mfano
                                                Umoja                                                                         wingi
                         Mu + tu (mtu)                                                                        watu
                         Mutoto (mtoto)                                                          watoto
                        Muungwana                                                                waungwana
                        Muana (mwana)                                                         wana
Mofu (MU) ya umbo halisi la umoja katika ngeli huweza kudhihirishwa katika maumbo mbalimbali kama vile {M, MU na MW}.
2)      Ngeli ya M-MI
Ngeli hii ina nomino ambazo hutumia kiambishi awali {M} katika umoja na {MI} katika wingi.
Kwa mfano;     umoja                                                  wingi
                                    M + ti                                                  mi + ti
                                    M + tume                                            mi + tume
                                    M + chungwa                                      mi + chungwa
                                    M +chezo                                            mi + chezo
3)      Ngeli ya JI-MA
Katika ngeli hii zipo nomino zilizo na kiambishi awali cha umoja {JI} na kiambishi awali cha wingi {MA}. Kwa mfano:
                                    Umoja                                                             wingi
                                    Jicho                                                    macho
                                    Jiwe                                                     mawe
                                    Jino                                                      meno
                                    Jiko                                                      maiko (meko).
4)      Ngeli ya KI-VI
Katika ngeli hii zipo aina za nomino zilizo na kiambishi awali cha umoja {KI} na kiambishi awali cha wingi {VI}. Kwa mfano:
                                    Umoja                                                             wingi
                                    Kiti                                                       viti
                                    Kiatu                                                    viatu
                                    Kiumba (chumba)                               viumba (vyumba)
                                    Kiakila (chakula)                                 viakula (vyakula).
Hapa umbo {KI} kiambishi awali cha umoja, lina alomofu mbili yaani {Ki} na {Cha} na umbo {VI} la wingi lina alomofu {Vi} na {Vy}.
5)      Ngeli ya U-N
Katika ngeli hii kuna nomino zenye kiambishi awali {U} umoja na {N} wingi. Kwa mfano:
                                    Umoja                                                             wingi
                                    Udevu                                                  ndevu
                                    Udago                                                  ndago
                                    Udara                                                  ndara
                                    Ulimi                                                   ndimi
                                    Ubawa                                                 mbawa
Tunaona hapa kuwa {N} umbo la wingi lina alomofu mbili yaani {N} na {M} katika muktadha maalumu.
6)      Ngeli ya U-MA
Katika ngeli hii {U} ni kiambishi cha umoja na {MA} ni kiambishi cha wingi. Kwa mfano:
                                    Umoja                                                             wingi
                                    Ugonjwa                                              magonjwa
                                    Uasi                                                     maasi
                                    Upishi                                                  mapishi
                                    Uamuzi                                                maamuzi.
7)      Ngeli ya U- Ø 
Ngeli hii hujumuisha maneno ambayo kiambishi awali umoja huwa ni {U} na kiambishi awali wingi mofu kappa{ Ø}. Kwa mfano:
                                    Umoja                                                             wingi
                                    Ukuta                                                   Ø + kuta (kuta)
                                    Ukucha                                                Ø + kucha (kucha)
                                    Upande                                                Ø + pande (pande).
8)      Ngeli ya Ø-MA
Katika ngeli hii mofu kappa { Ø} huwakilisha umoja na mofu {ma} huwakilisha wingi. Kwa mfano:
                                    Umoja                                                             wingi
                                    Ø debe                                                            madebe
                                    Ø kasha                                               makasha
                                    Ø jembe                                              majembe
                                    Ø bepari                                              mabepari.
9)      Ngeli ya Ø-Ø
Nomino zilizo katika ngeli hii ni zile ambazo hazina kiambishi idadi hata kimoja. Maumbo ya nomino hizi hayaoneshi idadi (umoja na wingi) katika maumbo yake. Kwa mfano:
                                    Umoja                                                 wingi
                                    Taa                                                      taa
                                    Saa                                                      saa
                                    Kuku                                                    kuku
                                    Ng’ombe                                             ng’ombe
                                    Nyumba                                               nyumba
                                    Samaki                                                            samaki.
Baada ya kuona uainishaji wa ngeli za nomino kwa kutumia kigezo cha kimofolojia kwa mujibu wa Mgullu, tutazame uainishaji wa ngeli hizi kwa kutumi kigezo hikihiki cha kimofolojia kwa mujibu wa Habwe na Karanja (2012). Wao wanaainisha ngeli za nomino kwa kuzingatia kufanana kwa viambishi vya mianzo ya nomino. Nomino zenye viambishi awali vilivyosawa huwekwa katika ngeli moja. Wao wanaainisha ngeli zifuatazo:
1.      Ngeli ya {MU}
Ngeli hii huchukua nomino zenye kiambishi ngeli {mu} pamoja na alomofu zake.
Kwa mfano; {MU} m- motto, mtu,
                             mu- muungwana, muuaji na
                             mw- mwalimu.
2.      Ngeli ya {WA}
Hii ni ngeli yenye kundi la wingi wa ngeli ya kwanza. Kwa mfano:
                        {WA} - watoto, watu, waungwana, wauaji na waalimu.
3.      Ngeli ya {M}
Ngeli hii ni ya umoja ambayo pia ina alomofu zake tatu yaani m, mu na mw. Kwa mfano:
                        Mut i- mti
                        Muembe - mwembe
                        Mundi – mundi.
{mw} hutokea ikiwa shina la nomino linaanzia na vokali [u], huwa {m} ikiwa shina la nomino linaanza na konsonanti na huwa {mu} ikiwa shina la nomino linaanza na vokali [u].
4.      Ngeli ya {MI}
Ngeli hii huchukua wingi wa ngeli ya tatu. Kwa mfano:
                        Miti, migomba, miembe na miundi.
5.      Ngeli ya {JI/Ø}
Mofu ya ngeli hii huwa ni {ji}. Kwa mfano jitu, jicho, Øgoti, na Øtawi. Kuna nomino zingine huunganishwa katika kundi hili japo hazina umbo dhahiri lililotajwa kwa maana zina mofu kapa. Nomino hizi huunganishwa katika kundi hili kwa sababu zenyewe wingi wake unaingiliana na ule wa kundi hili unaodhihirishwa katika ngeli ya sita.
6.      Ngeli ya {MA}
Ngeli hii huwakilisha wingi wa ngeli ya tano. Kwa mfano: macho, magoti, matawi na majitu.
7.      Ngeli ya {KI}
Mofu ngeli {ki} huwa na alomofu {ch} kutokana na kanuni za kifonolojia (ukaakaishaji). Kwa mfano nomino katika kundi hili ni: kiatu, kitu, kisu na kiakula (chakula).
8.      Ngeli ya {VI}
Ngeli hii huonesha wingi wa ngeli ya saba kwa mfano viatu, vitu, visu na viakula (vyakula). Ngeli hii ina alomofu {vy}.
9.      Ngeli ya {N/Ø}
Ngeli hii huhusisha majina yanayoanza na N na kufuatiwa na konsonanti. Kwa mfano nyumba, nguzo na nguo.
10.  Ngeli ya {N/Ø}
Ngeli hii huwakilisha wingi wa ngeli ya tisa {n} japokuwa hakidhihiriki kaika maneno mengi ya ngeli hii. Ngeli ya tisa na kumi hudhihirika zaidi kisintaksia na siyo kimofolojia tu.
11.  Ngeli ya {U}
Nomino zenye kiambishi cha umoja {u} kwa mfano ulimi na ugonjwa huingia katika kundi hili. Pia ngeli hii ina alomofu {w} kwa mfano maneno kama: uembe (wembe) na uaraka (waraka).
12.  Ngeli ya {KA} kwa mfano katoto na kagari.
13.  Ngeli ya {TU}
Ngeli hii inawakilisha wingi wa ngeli ya 12. Kwa mfano: tu + toto na  tu + gari. Pia ngeli hii huwa na alomofu {tw}. Kwa mfano: twana na twalima (tuana na tualima).
14.  Ngeli ya {U} kwa mfano u + zuri na u + tukufu.
15.  Ngeli ya {KU}
Ngeli hii hurejelea vitenzi vinavzofanya kazi kama nomino. Kwa mfano: kuimba, kucheza na kuruka.
16.  Ngeli ya {PA}
Ngeli hii huonesha mahali kamili au mahususi kwa mfano: pale, ndani na hapa.
17.  Ngeli ya {KU}. Ngeli hii huonesha mahali kwa ujumla kwa mfano huku.
18.  Ngeli ya {MU}. Ngeli hii huonesha undani wa mahali kwa mfano humu, na mule.
Baada ya kuona uainishaji wa ngeli za nomino kwa kutumia kigezo cha kimofolojia kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali, ufuatao ni upungufu wa kigezo hiki:

Muingiliano wa ngeli kwa mfano ngeli ya 1. Umoja na ya 2. Umoja ambapo kiambishi au mofu yake ni {m}. Kwa mfano katika maneno kama vile: mtu, mwana, mtoto na muungwana katika ngeli ya kwanza umoja na mti, mtume, mchungwa na mkono katika ngeli ya pili. Hali hii ya muingiliano inatokea pia katika ngeli ya 3 na 6 wingi, na ngeli ya 5, 6 na 7 umoja. Hii ni kwa mujibu wa mgullu (2001).
Kuna baadhi ya ngeli zinaonesha kiambishi kimoja tu aidha cha wingi au umoja. Kwa mfano kwa mujibu wa uainishaji wa Mgullu (2001) katika ngeli ya 7. {U- Ø} na ngeli ya 8. { Ø-MA}. Ngeli hizi hazina viambishi vya upande mmoja kwa mfano katika ngeli ya saba wingi na ngeli ya nane umoja.
Ngeli ya 9. (Ø - Ø) kwa mujibu wa mgullu (2001) haina kiambishi chochote aidha cha umoja au wingi. Huu ni udhaifu mwingine kwa kua msingi wa uainishaji huu (uainishaji wa kimofolojia) huzingatia viambishi awali vya umoja na wingi katika nomino ambavyo hufanana na kisha kuziweka  nomino hizo pamoja katika ngeli moja.
Uainishaji huu unachanganya nomino zisizo na uhai na zile zenye uhai. Kwa mfano kwa mujibu wa Mgullu (keshatajwa), katika ngeli ya nne kuna majina ya viumbe wenye uhai na vitu visivyo na uhai kwa mfano: kiti/viti, kiatu/viatu na kiumba (chumba)/viumba (vyumba) hizi ni nomino za vitu visivyo na uhai. Kwa upande mwingine nomino za vitu vyenye uhai ambazo huwekwa katika kundi hili ni kama vile: kiongozi/viongozi, kipofu/vipofu, kilema/vilema na kijana/vijana.
Kigezo hiki kinajihusisha na maumbo ya umoja na wingi tu na kutupilia mbali upatanisho wa kisarufi.
Pia udhaifu mwingine wa uainishaji wa ngeli za nomino kwa kutumia kigezo hiki cha kimofolojia, wataalamu wanatofautiana katika idadi ya ngeli. Kwa mfano Mgullu (keshatajwa) anaainisha ngeli tisa wakati Habwe na Karanja (wameshatajwa) wanaainisha ngeli kumi na nane.


MAREJELEO

Habwe, J. & Karanja, P. (2012). Misingi ya Sarufi ya Kiswahili. Nairobi: Phoenix Publishers.
Mgullu, R.S. (2001). Mtalaa wa isimu. Nairobi: Longhorn Publishers Ltd.

Tuesday, May 26, 2015

DHANA YA NENO

DHANA YA NENO NI TATA

Na Mwl.  CLEMENT, D.L



SWALI:  Baadhi ya wanaisimu wanakubaliana kwamba dhana ya neno ni tata. Pinga au kubali
                kauli hii kwa hoja madhubuti.


Katika kueleza dhana ya neno ni vyema  tukaanza na kutazama dhana ya mofolojia kwa ufupi. Dhana ya mofolojia imeelezwa na wataalam mbalimbali na miongoni mwao ni:
Habwe na Karanja (2012) wanadai kuwa mofolojia ni neno linalotumiwa kumaanisha utanzu wa isimu unaoshughulikia muundo wa maneno.
Hartman (1972) anaeleza kuwa mofolojia ni tawi la isimu ambalo hushughulikia uchunguzi na uchambuzi wa maumbo na aina za maneno yaliyo pamoja na historia zake.
Hivyo baada ya kuona fasili hizo kulingana na wataalamu mbalimbali, mofolojia yaweza kufasiliwa kama taaluma ya isimu inayojishughulisha na uchunguzi, uchambuzi na ufafanuzi wa maumbo ya maneno. Baada ya kuona fasili mbalimbali za mofolojia kulingana na wataalamu mbalimbali na kisha kuona fasili ya ujumla, sasa kwa ufupi tuitazame dhana ya neno. Dhana ya neno imefasiliwa na wataalamu mbalimbali na miongoni mwao ni hawa wafuatao:
Mdee (2010) anaeleza kuwa neno ni mfululizo wa herufi zilizofungamana pamoja na kuzungukwa na nafasi tupu.
Rubanza (2010) anadai kuwa neno kiothografia ni mfuatano wa maandishi ambao huacha nafasi tupu mwishoni bila uwepo wa nafasi tupu katikati.
Katamba (1994) anaeleza kuwa neno ni kipashio kidogo cha maana katika lugha ambacho kina dhima ya kisarufi. Anaendelea kusema, neno linaweza kusimama pekeyake na kuleta maana bila kupachikwa vipande vingine.

Ni kweli kuwa dhana ya neno ni tata katika kuifasili. Utata huu unatokana na vigezo mbalimbali vya kisarufi ambavyo wanaisimu huvitumia kama mwongozo katika kufasili dhana hii. Miongoni mwa vigezo hivyo ni kama ifuatavyo:

Wanaisimu wanatumia kigezo cha kiothografia. Katika kigezo hiki, huchukulia dhana ya neno kuwa ni maandishi yanayoacha nafasi mwisho. Neno hudhihirika katika maandishi tu na lisiwe na nafasi katikati. Kwa mfano Rubanza (2010) anaeleza kwamba neno kiothografia ni mfuatano wa maandishi ambao huacha nafasi tupu mwishoni bila uwepo wa nafasi tupu katikati. Kwa mfano katika sentensi; baba analima shambani. Katika mfano huu, sentensi tajwa ina maneno matatu yaliyopigiwa msitari. Kigezo hiki kina changamoto zifuatazo:
Kigezo hiki huchukulia maneno ambatani kuwa ni maneno tofauti kwa kuwa baadhi yake huandikwa kwa kuacha nafasi tupu katikati. Dai hili sio kweli kwasababu maneno ambatani hurejelea dhana moja hivyo hupaswa kuchukuliwa kama neno moja. Kwa mfano maneno kama: bata mzinga na bwana misitu.
Nafasi tupu huonekana katika maandishi tu (lugha ya maandishi) na hivyo kwa kiasi kikubwa kigezo hiki kimejikita zaidi katika lugha ya maandishi na kutupilia mbali lugha ya mazungumzo kwani tunapoongea nafasi tupu huwa hazionekani. Hali hii inapelekea kujiuliza maswali kama, je neno ni lile lililoandikwa tu?

Wanaisimu wanatumia kigezo cha kimofolojia. Katika kigezo hiki huchukulia kuwa, neno ni kipande cha lugha kinachotokana na kujengwa na kipashio kidogo cha kimatamshi kufuatana na vigezo au utaratibu fulani uliowekwa. Utaratibu huo hutofautiana kutoka lugha moja na nyingine. Kwa mfano Rubanza (2010) anaeleza kwamba zipo lugha ambazo upo uwezekano wa kulitambua neno kwa kutumia sifa za kimatamshi. Lugha kama hizi ni zile ambazo zina utaratibu wa kuweka mkazo mahali fulani maalumu katika maneno wakati wote. Anaeleza zaidi kwamba sehemu hiyo inaweza kuwa mwanzoni mwa kila silabi ya kwanza ya neno au silabi ya pili toka mwisho kwa baadhi ya lugha. Kwa mfano katika lugha ya Kiingereza sentensi “ I didn’t take the test yesterday”. Kutokana na utaratibu wa lugha hii ambapo mkazo huwekwa katika maneno yenye kubeba maana ya msingi (content words), sentensi hii ina maneno matatu yaliyokolezwa.
Utaratibu huu si mara zote kwani kuna wakati mwingine kutokana na sababu za kimsisitizo, maneno yanayobeba maana za kisarufi (grammatical words) huwekewa mkazo. Kwa mfano katika sentensi ileile mkazo ukiwekwa katika ‘I’ huonesha msisitizo kuwa sio yeye, ‘didn’t’ hakufanya na ‘the’ husisitiza jaribio hilo linalokusudiwa na muulizaji. Katika lugha ya Kiswahili mkazo huwekwa katika silabi ya pili kutoka mwisho. Kwa mfano ana'cheza, ana'lima na ana'kula.
Kigezo hiki kinasaidia kutofautisha maneno kwa kutumia mkazo hususa ni katika lugha ambazo mkazo huwa na uamilifu wa kubadili maana au kategoria ya neno. Kwa mfano katika lugha ya Kiingereza maneno kama: 'respect (nomino), res'pect (kitenzi) na 'record (nomino), re'cord (kitenzi) . Pia kigezo hiki kinatambua maneno katika lugha ya mazungumzo. Pamoja na ubora huu kigezo hiki kinakumbana na changamoto kadha. Miongoni mwa changamoto hizo ni:
Kigezo hiki kinashindwa kuweka bayana neno hasa ni lipi kwani tunaona kuna baadhi ya vipande-lugha visivyobeba maana ya msingi kama vile viunganishi na vihusishi katika lugha ya Kiswahili ambavyo haviwekewi mkazo. Swali ni kwamba, je vipande lugha hivyo ni maneno au si maneno?

Wanaisimu wanatumia kigezo cha kilekisika. Hiki ni kigezo kingine kinachotumiwa na wanaisimu kufasili dhana ya neno. Katika kigezo hiki, hueleza kuwa neno ni kipashio dhahania cha kilekisika ambacho huweza kudhihirika kimaana na kikazi. Kipashio hiki huweza kuwakilishwa kimaandishi au kimatamshi. Kwa mfano Mdee (2010) akimrejelea Crystal (1980) anaeleza kuwa leksimu ni kipashio dhahania kinachowakilisha maumbo kadhaa yanayotokana nacho. Kwa mfano: REFU- ndefu, mrefu, na kirefu. Kigezo hiki kina changamoto zifuatazo:
Hakiweki bayana juu ya maumbo yanayotokana na leksimu moja (midhihiriko ya hiyo leksimu) kuwa ni maneno tofauti au ni neno moja.
Kuna maneno yenye umbo moja lakini huwa na maana tofauti, je nayo yatakuwa ni neno moja au ni maneno tafauti? Kwa mfano maneno kama:
                      Paa        la nyumba (sehemu ya juu ya nyumba)
                                    mnyama
                                    enda juu au angani.
                        Mbuzi              mnyama
                                                kifaa cha kukunia nazi. 
  
Kigezo cha maana pia ni kigezo kingine ambacho wanaisimu mbalimbali hukitumia katika kufasili dhana ya neno. Katika kigezo hiki wanaisimu husisitiza maana katika kufasili dhana hii kwa kudai kuwa neno ni lazima liwe na maana. Kwa mfano Mdee (2010) anaeleza kwamba neno ni kipashio kidogo cha lugha chenye maana. Anaeleza zaidi kwamba neno ni lazima liwe na maana. Kwa mfano:  baba –  mzazi wa kiume, na mama – mzazi wa kike. Kigezo hiki pia kinakumbana na changamoto na miongoni mwa changamoto hizo ni kama ifuatavyo:
Kigezo hiki hakibainishi kuwa ni maneno yapi hulengwa hasa kwani kwa kiasi kikubwa kinaonekana kuegemea zaidi katika maana ya kilekisika na hivyo kuyasahau maumbo yenye maana za kisarufi kama vile viunganishi na vihusishi katika lugha ya Kiswahili.
Hakiweki wazi juu ya maneno yenye maana ya mficho kwa mfano nahau ambazo huundwa na umbo zaidi ya moja ilihali yakirejelea dhana moja. Kwa mfano:
                        mkono wa birika – mchoyo
                        pata jiko – kuoa.
Pia yapo maneno yenye maana zaidi ya moja kama vile: kaa, paa na kata. Maneno haya yakisimama pweke (peke yake), huwezi kupata maana moja hivyo ni lazima yawe katika mahusiano na maneno mengine matika mfumo wa matumizi katika sentensi ndipo upate maana. Mbali na kuwa katika mahusiano na maneno mengine katika sentensi, ni  muhimu pia kuzingatia muktadha ili kupata maana au dhana kamili ya maneno hayo.

Pia kigezo cha kisarufi ni miongoni mwa vigezo wanavyotumia wanaisimu katika kufasili dhana ya neno. Kwa mfano katamba (1994) anaeleza kuwa ili neno litambulike ni lazima liwe katika muktadha wa matumizi. Anaendelea kusema kuwa pia neno moja linaweza kuwa na dhima mbalimbali na dhima hizo hutambulika tu litakapokuwa ndani ya muktadha wa matumizi kwenye sentensi. Katamba (ameshatajwa) anatoa mfano wa neno la kiingereza ‘cut’ kwamba likiwa kiupweke, huwezi kutambua linarejelea nini. Neno hili linaweza kurejelea dhana tofauti linapokuwa katika mfumo. Kwa mfano;
i)                    ‘I need my cut’  nahitaji stahiki yangu (tafsiri ni yetu)
ii)                  ‘I have cut my finger’ nimekata kidole changu (tafsiri ni yetu)
Katika mifano hapo juu tunaona kuwa neno ‘cut’ katika sentensi ya kwanza limetumika kama nomino na katika sentensi ya pili kama kitenzi. Pia kigezo hiki kinaenda mbali zaidi katika kufafanua maumbo kama: na, tu na si (katika Kiswahili) na maumbo kama: and, an, the, na on (katika lugha ya Kiingereza) kuwa hutambulika yanarejelea nini au yana maana gani yakiwa katika muktadha wa matumizi.
Changamoto ya kigezo hiki ni kwamba si lazima maneno yote yawe katika muktadha wa matumizi ndipo tuweze kubaini maana zake kwani kuna baadhi ya maneno huweza kutambulika kuwa yana maana gani hata yasipokuwa katika muktadha  wa matumizi katika sentensi. Kwa mfano nomino za mahali kama vile: Dodoma, Mwanza na Morogoro na majina ya watu kama vile: Amina, Omari, Fatuma na Ali.

Mbali na vigezo wanavyovitumia wanaisimu katika kufasili dhana ya neno, wanakubaliana kuwa dhana ya neno ni tata hata katika uainishaji wa aina za maneno kiidadi na istilahi wanazozitumia. Kwa mfano katika kigezo cha idadi, Nkwera (1989) na Kapinga (1983) wanaainisha aina saba za maneno wakati Kihore (1969) anaainisha aina nane za maneno. Pia kiistilahi Nkwera (ameshatajwa), anatumia istilahi nomino wakati Kihore na Kapinga (wameshatajwa), wanatumia istilahi majina kurujelea dhana ileile.

Kwa kuhitimisha, katika kufasili dhana ya neno ni vyema kuzingatia vigezo vyote vya kisarufi kama vile othografia, fonolojia, sarufi, maana na lekisika ili kupunguza changamoto zinazojitokeza katika kufasili dhana hii kama ilivyojibainisha hapo juu. Hivyo kulingana na vigezo tajwa hapo juu dhana ya neno yaweza kufasiliwa kama kipashio cha lugha kilichojengwa na vipande sauti mbalimbali vya matamshi, chenye maana aidha ya kilekisika au ya kisarufi, kinachoweza kujibainisha kimaandishi na kimatamshi na kuwa na uwezo wa kuchukua sifa mbalimbali kinapokuwa katika muktdha wa matumizi.




MAREJEO
Habwe, J. & Karanja, P. (2012). Misingi ya Sarufi ya Kiswahili. Nairobi: Phoenix Publishers.
Katamba, F. (1993). Morphology. London: MacMillan Press Ltd.
Mdee, S. (2010). Nadharia na Historia ya Leksikografia. Dar es Salaam: TUKI.
Nkwera, F.V.M. (1989). Sarufi na Fasihi Sekondari na Vyuo. Dar es Salaam: Printpak.
Rubanza, (2010). Basic Reading.